Monday, 3 April 2017

WATOTO WAZUIWA KWENDA SHULE KUHOFIA KUPATA MIMBA

Kutokana na tatizo la upungufu wa walimu katika Shule ya Msingi Mbalawala Manispaa ya Dodoma,
wazazi wa watoto wanaosoma shuleni hapo wamewazuia watoto wao kwenda shule kuanzia leo hadi hapo watakapopelekewa walimu wa kutosha.

Wazazi hao walichukua uamuzi huo katika mkutano wa kijiji na kamati ya shule hiyo, uliofanyika shuleni hapo mwishoni mwa wiki.

Shule hiyo ina walimu watano tu wanaohudumia mikondo saba.

Wakizungumza katika mkutano huo wazazi hao walisema kuwa, wameamua kuchukua uamuzi huo kwa kuhofia watoto wao kupata mimba za utotoni kutokana na kukosa uangalizi wa walimu wakiwa shuleni.

Mkazi wa kijiji hicho Hamis Sanda amesema shule hiyo ya muda mrefu ina walimu wachache, na kila mara wamekuwa wakiahidiwa kupelekewa walimu, lakini hakuna utekelezaji unaofanyika hali inayosababisha wanafunzi kushindwa kusoma.

Alisema wamechoshwa kuona watoto wao wakienda shule lakini hawajui chochote kutokana na kutofundishwa na wengi wao waliopo darasa la saba, hawajui kusoma wala kuandika.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment