Kiongozi wa
Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee
(Chadema), jana wamehojiwa na Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge kwa
muda wa saa mbili – saa moja kila mmoja.
Wamehojiwa na
kamati hiyo baada ya saa 48 tangu Spika wa Bunge, Job Ndugai, atoe agizo la
kumtaka Mdee afike bungeni ndani ya saa 24 vinginevyo akamatwe na polisi.
Kuhojiwa kwa
wanasiasa hao, kulithibitishwa na Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Bunge,
Owen Mwandumbya.
Hata hivyo, Owen
alisema hawezi kuzungumza yaliyojiri ndani ya kikao hicho kwa kuwa hakuingia.
Kwa upande wake,
Mbowe alisema kamati hiyo ilimuhoji juu ya kauli nne alizotoa usiku wa Jumanne
ya wiki hii mbele ya waandishi wa habari, baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa
wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), ambao wagombea wawili wa Chadema,
Lawrence Masha na Ezekia Wenje, walipigiwa kura za hapana.
Mbowe alisema
kauli hizo ni pamoja na aliyosema Ndugai amevunja kanuni na sheria hazikufuatwa
katika uchaguzi huo, mchakato wa uchaguzi huo ulikuwa ni mkakati wa Serikali na
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alikuwa anajua, wagombea Chadema walikuwa wazuri
lakini kupigwa kura ya hapana ilikuwa ni mkakati wa CCM na ya nne uchaguzi
ulikuwa batili.
Naye Mdee
alisema alihojiwa juu ya tuhuma zilizotolewa na Ndugai kwamba alitoa kauli za
matusi bungeni na suala la pili ni kuzungumza bungeni bila kupewa ruhusa ya
Spika.
0 comments:
Post a Comment