Ripoti mpya kuhusu hali ya janga la chakula duniani imesema idadi
ya watu wasio na uhakika wa kupata chakula iliongezeka mwaka jana na kufikia
watu milioni 108,
ikilinganishwa na milioni 80 mwaka 2015, licha ya jitihada za
kimataifa za kuhakikisha watu wana chakula cha kutosha. Taarifa kamili na Flora
Nducha.
Ikiwa imeandaliwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa kama lile la
chakula, FAO na wadau wao ukiwemo Muungano wa Ulaya na shirika la maendeleo ya
kimataifa la Marekani, USAID, ripoti imetolewa leo huko Brussels, Ubelgiji
ikisema idadi hiyo inagusa tu watu ambao hali zao ziko taabani zaidi.
Kichocheo kikubwa cha ukosefu wa chakula ni mizozo ambapo ripoti
imesema kuwa nchi 10 kati ya 13 zinazokabiliwa na njaa ya kupindukia ni zile
zenye migogoro kama vile Somalia, Sudan Kusini na Nigeria.
Luca Russo, mshauri mwandamizi kutoka FAO amesema ripoti hii ni
muhimu sana kwa kuwa imejumuisha mashirika yote yanahusika na usaidizi kwenye
janga la chakula.
Ripoti inaeleza kuwa muda unasonga na hivyo jamii ya kimataifa
ichukue hatua kuokoa maisha ya mamilioni ya watu walio kwenye hatari ya
kukumbwa na njaa.
0 comments:
Post a Comment