Monday 11 May 2015

Sheria ya makosa ya mitandao tayari imesainiwa na Rais…!!!!



Rais Jakaya Kikwete tayari ameshasaini sheria yenye utata ya makosa ya mtandao na muda wowote kuanzia sasa itaanza kutumika rasmi.

Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, amesema hayo leo wakati akizungumzia masuala mbali mbali yanayohusu sheria hiyo ambayo kupitishwa kwake kumesababisha malalamiko mengi kutoka kwa wadau kuwa itaminya uhuru wa habari, kuingilia faragha pamoja na uhuru wa watu kuwasiliana.
Ufuatao hapa chini ni uchambuzi kidogo kuhusu baadhi ya vipengele vilivyozua utata katika muswada huu uliokuwa umetolewa
1. Kifungu 7 (2b): Mpokeaji wa ujumbe (receiver) anaweza kushtakiwa kwa kosa la kupokea ujumbe ambao sheria imeufanya kuwa wa jinai. (Mfano: Mtu akikuforwadia ujumbe, ukiupokea na wewe umefanya kosa la jinai).
2. Kifungu 8: Itakuwa ni kosa la jinai kama mtu ataweka wazi nyaraka za siri za serikali hata kama ni nyaraka ya kusaidia nchi kwa ujumla (Mfano: Matumizi mabaya ya mali ya umma).
3. Kifungu 14: Picha yoyote yenye mwelekeo unaoweza kuonekana kama ‘mchafu kingono’ inaweza kupelekea mtu kufungwa hadi miaka 10 au kulipa milioni 30; (Mfano: mtu kaposti picha yake ambayo sio ya ponografia lakini ‘ikatafsiriwa’ hivyo. Sheria haijatafsiri ponografia!)
4. Kifungu 23: Je, ulijua kuwa ‘kusababisha maudhi ya hisia’ kwa mtu mwingine ni unyanyasaji na unaweza kufungwa kifungo kisichopungua mwaka mmoja?
5 Kifungu 22: Ukiweka ujumbe katika mtandao na ukaufuta au kuuboresha, kama ukishtakiwa kwa kuweka ujumbe huo unaweza kuhukumiwa pia kwa adhabu ya kuuboresha au kuufuta. (Mfano: unapofuta ‘status’ zako za WhatsApp, unaweza shitakiwa kwa kuchelewesha ushahidi kisa tu ulifuta na hamna mtu anayeweza kujua ulifuta kwa kusudi au la.)
6. Mkuu wa kituo cha Polisi chochote kile nchini anaweza kuagiza wewe umpatie simu/laptop yako au taarifa zako zote (kwenye email, chats) au hata vifaa vyako au ofisi yako kwa ajili ya upelelezi bila oda ya Mahakama.
7. Serikali kupitia waziri husika ndio ina mamlaka ya kusema jambo lililowekwa kwenye mtandao ni la kweli, uongo au la kupotosha

0 comments:

Post a Comment