Ripoti ya awali ya Utoaji wa Huduma za
Kipolisi (PDB) inayosimamia usalama wa raia na
mali zao, inaonyesha Mkoa wa
Kipolisi wa Kinondoni unaongoza kwa vitendo vya uhalifu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa
ripoti hiyo tarehe 18 feb 2016 jijini Dar es Salaam Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP
Ernest Mangu, alisema ripoti hiyo imetolewa ili kupanga mikakati mipya ya
kupambana na vitendo vya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwamo
Kinondoni.
Alisema kutokana na hali hiyo,
jeshi hilo limejipanga kuhakikisha vitendo hivyo vinakwisha ili wananchi waishi
kwa amani na utulivu.
Aliongeza kuwa hadi sasa
wamefungua vituo vya kanda za kipolisi 37 maeneo mbalimbali ya mkoa huo ambavyo
vitakuwa na askari wa kutosha, ambao watakuwa na silaha kwa ajili ya kufanya
doria.
Alisema askari hao watakuwa tayari
kupambana na uhalifu wa aina yoyote utakaojitokeza.
Mangu alisema ripoti hiyo
imetolewa chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ambao unahitaji
kutekelezwa kwa vitendo.
Aliwataka askari wa jeshi hilo
kila mmoja kutimiza majukumu yake kulingana na nafasi yake ili waweze kupambana
na uhalifu.
Alisema endapo Serikali itatoa
fedha za kutosha, kazi hiyo itaendelea katika mikoa mingine ya kipolisi ya
Ilala na Temeke na baadae kusambaa nchi nzima.
0 comments:
Post a Comment