Basi
linalotumia umeme wa nguvu za jua ambalo watengezaji wake toka Uganda wanadai kuwa
la kwanza barani Afrika, limeendeshwa hadharani.
Basi hilo la kielektroniki aina
ya Kayoola linalomilikiwa na kampuni ya Kiira Motors, lilionyeshwa katika
uwanja wa Uganda mjini Kampala.
Mojawapo ya betri zake zinaweza
kuwekwa chaji na vibamba vya umeme wa jua katika paa la nyumba, ambavyo
huongeza kasi ya gari hilo hadi kilomita 80 kwa saa.
Watengezaji wake sasa wanalenga
kuwavutia wateja wataolitengeza basi hilo,ili kuvutia soko kubwa la magari
duniani.
Mkurugenzi mkuu wa Kiira Motors
Paul Isaac Musasizi, amesema kwamba amefurahishwa na jaribio la gari hilo
lilipoendeshwa.
Raia wamefurahishwa na wazo
kwamba Uganda ina uwezo wa kutengeza mfano kama huu, na bw. Musasizi anasema
kwamba angependelea kulisaidia taifa hilo kushindana na kampuni nyengine za
magari katika eneo hili.
Pia anatumai kwamba hatua hiyo
itabuni ajira zifikiazo 7000 kufikia mwaka 2018.
Hatahivyo mradi huo hauwezi kuanza bila ya usaidizi wa
kampuni zinazotengeza vifaa vya magari.
Lengo ni kwamba kufikia 2039 kampuni hiyo itakuwa na
uwezo wa kutengeza vifaa vya magari na kuviunganisha nchini Uganda bila
kutegemea kampuni nyengine .
Basi hilo lenye viti 35 linalenga
kufanya kazi katika miji midogo badala ya mji mkuu kutokana na masharti ya
umbali linakoweza kusafiri.
Iwapo mabasi hayo yatazalishwa
kwa wingi, kila basi litagharimu kiasi cha dola 58,000 ambacho bw Musaizi
anasema ni bei nzuri katika soko lenye ushindani mkubwa.
Kampuni ya Kiira Motors
ilianzishwa kutokana na mradi uliofanyika katika chuo kikuu cha Makerere, ambacho
ni mmoja wa mmiliki wa hisa katika kampuni hiyo na pia kimenufaika na ufadhili
kutoka kwa hazina ya fedha ya serikali.
0 comments:
Post a Comment