Thursday 21 April 2016

WANANE MBARONI KWA KUNYWA POMBE MCHANA…

Wilaya ya Sengerema imeanza kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais, baada ya kukamata watu wanane waliokutwa wakinywa pombe saa za kazi.

Amri ya kukamatwa na kuwekwa mahabusu kwa watu hao ilitolewa juzi na Mkuu wa Wilaya Zainabu Terack, baada ya kukuta baa zimefunguliwa asubuhi zikiwa na wateja waliokuwa wakipata kinywaji kabla ya saa 9:30 alasiri, muda ambao ofisi za Serikali hufungwa.
Rais John Magufuli alitoa agizo hilo la kupiga marufuku unywaji pombe na uchezaji pool nyakati za kazi, wakati alipokuwa akiwaapisha wakuu wa mikoa mwezi uliopita.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya aliyeongoza oparesheni ya dakika 45 ya kusaka wanaokunywa pombe na kucheza pool muda wa kazi, watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kwa makosa ya uzembe na kukiuka amri halali ya serikali.
Wakijitetea baada ya kutiwa mbaroni baadhi ya waliokamatwa, walidai kuwa walienda baa kujiliwaza wakati wa msiba wa ndugu yao waliyemtaja kwa jina la Petro Shoyo, na kumwomba mkuu wa wilaya kuwasamehe kwa sababu ni kosa lao la kwanza.
Lakini mkuu huyo wa wilaya alisisitiza wapelekwe mahakamani.

0 comments:

Post a Comment