Katika karibu kila jambo duniani, mwanadamu huhitajika kutumia akili ili
kufanikiwa.
Bila shaka iwapo utatarajia uwazidi watu wengine hasa katika kuwapora au
kuwaibia basi utahitajika kuwa na ujanja zaidi.
Lakini maeneo mbalimbali duniani kunao wahalifu ambao walionekana
kupungukiwa ujanja.
Majuzi kwa mfano
wanaume wawili kutoka Skegness Lincolnshire, walijipiga picha wakiimba pesa
kutoka kwenye mitambo ya kucheza Kamari Bradford, Uingereza.
Hawakuenda mbali kwani
walikamatwa muda mfupi baadaye Benjamin Robinson 30, alifungwa jela miezi 32
naye Daniel Hutchinson,akahukumiwa kifungo cha miezi sita jela ambacho
kimeahirishwa.
Hao hawako peke yao
hapa nimekuwekea listi ya wahalifu wengine waliojichongea:
1. Jambazi aliyejitapa Facebook
Andrew Hennells
alikamatwa baada ya kuandika kwenye Facebook akijisifu kuhusu mpango wake wa
kushambulia duka la jumla la Tesco eneo la King's Lynn Norfolk.
Aliweka kwenye
Facebook picha yake ya kujipiga yaani ‘selfie’, picha ya kisu na kuandika:
"Doing Tesco Over." (Nafanya Tesco Twende).
Alikamatwa na polisi
dakika 15 baadaye akiwa na kisu chake na pesa £410 alizoiba.
Alifungwa jela miaka
minne Aprili mwaka jana.
2. Mwizi aliyetekwa na usingizi
Wachumba katika eneo
la Lancashire walirejea kutoka likizoni mwaka 2014 na kumpata mwizi amelala
usingizi wa pono katika kitanda chao.
Martin Holtby and Pat
Dyson walishangaa kumpata mwizi huyo Lukasz Chojnowski, alikuwa ameosha vyombo,
akafua nguo zake za ndani na hata kununua mboga.
Wanasema nyumba yao
haikuwa safi sana walipoondoka kwenda likizoni.
Walimpata Chojnowski
aliyetoka Poland lakini akahamia Leeds, alikuwa amefanya usafi vilivyo.
Chojnowski 28 alikiri
kosa la kuvunja nyumba na akatakiwa kukaa miaka miwili bila kutenda kosa na
kulipa gharama ya £200.
3. Mwizi wa benki aliyeacha anwani yake
Mwizi wa benki
aliyejaribu kujificha kwa kuvalia miwani ya giza n ahata kuvalia soksi juu ya
viatu vyake, alisahau kwamba alikuwa ameacha anwani yake.
Dean Smith 27 alikuwa
ameenda kwenye tawi la benki ya Barclays eneo la Treorchy, Wales kubadilisha
anwani yake alipovutiwa na pesa zilizokuwa kwenye meza.
Alirejea baadaye akiwa amevalia miwani hiyo ya giza na
soksi na kumtaka keshia ampe pesa hizo.
Keshia alikataa na akalazimika kutoroka mikono mitupu.
Polisi walimpata kwa njia rahisi baada ya kufuatilia video ya kamera ya CCTV,
wakamtambua na kisha kufahamu anwani yake.
Alikiri kwamba alikuwa “mjinga
sana” na alifungwa miaka miwili unusu.
4. Mwizi aliyewatumia polisi picha nzuri
Mwanamume aliyekuwa
akisakwa kwa makosa ya kuteketeza na kuharibu mali alituma picha ya selfie kwa
maafisa wa polisi akisema picha iliyotumiwa na maafisa hao katika tangazo la
kutafutwa kwake haikuwa ya kupendeza.
Donald "Chip" Pugh aliwatumia maafisa wa polisi
picha aliyojipiga mwenyewe na kuandika ujumbe unaosema: "Hii hapa picha
yangu nzuri, hiyo mliyotumia ni mbaya sana”.
Polise katika mji wa Lima jimbo
la Ohio, walikuwa wamepakia picha kwenye ukurasa wao wa Facebook wakiomba
msaada wa kumtafuta Bw Pugh.
Polisi walimjibu na kusema
angefanya hisani zaidi kwa kujifikisha kwao,hata hivyo alikamatwa baadaye katika
jimbo la Florida.
5. Gaidi aliyejitokeza kudai zawadi
Maafisa nchini Afghanisan
waliachwa vinywa wazi baada ya kamanda mmoja wa kundi la Taliban kujisalimisha
na kisha kujaribu kudai zawadi ya $100 iliyokuwa imeahidiwa mtu ambaye angesaidia
kukamatwa kwake.
Mohammad Ashan alituhumiwa kupanga mashambulio dhidi ya
wanajeshi wa Marekani na Afghanistan mashariki mwa nchi hiyo.
Ripoti zinasema alifika katika
kizuizi cha polisi mwaka 2012, akaelekeza mkono wake kwenye bango lenye picha
yake na kisha akadai zawadi hiyo ya $100.
Maafisa wa usalama walishangaa
sana na kushindwa kuelezea kitendo chake. Afisa mmoja wa Marekani anadaiwa kuambia
wanahabari: “Kusema kweli, mwanamume huyu ni mpumbavu.”
0 comments:
Post a Comment