Mlima Kilimanjaro umeendelea kuipaisha Tanzania kimataifa, baada ya
kushinda kivutio cha asili Afrika kwenye Tuzo za Utalii duniani (WTA)
zilizofanyika juzi visiwani Zanzibar.
Mlima huo ni moja ya vipengele sita
ambavyo Tanzania ilishinda, baada ya kugombea vipengele ishirini kati ya zaidi
ya 1,200 vilivyokuwa vinashindaniwa na nchi za Afrika na Bara Hindi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Rais wa WTA Graham Cooke, amewapongeza washindi wa tuzo
hizo na kuwataka kujenga mtandao utakaokuza utalii kwa nchi pamoja na wadau
mbalimbali wa sekta hiyo.
Wakati mlima huo ukishinda kipengele
cha kivutio bora Afrika, tuzo nyingine zilienda kwa Four Seasons Safari Lodge
Serengeti ikiwa ni hoteli bora ya mbugani, Beyond Mnemba Island Lodge ya
Zanzibar iliyoibuka hoteli bora ya kisiwani.
Nyingine ni Singita Sasakwa Lodge iliyoshinda kuwa hoteli ya
kifahari Afrika na hoteli yalipofanyika maonyesho hayo, Diamonds La Gemma
dell’Est ikiwa ni hoteli bora ya ufukweni.
Fastjet imeibuka kuwa ndege yenye gharama za chini zaidi Afrika.
Meneja Mkuu wa Diamonds La Gemma
dell’Est, Andrew Cook aliishukuru WTA kwa kuipa heshima ya pekee Tanzania
kuandaa na kusimamia tuzo hizo na kuichagua hoteli yake kati ya nyingi zilizopo
nchini.
Washindi wengine wa jumla walikuwa
Hoteli ya Serena iliyoibuka kidedea kwa hoteli bora Afrika wakati Shirika la
Ndege la Kenya likiwa kinara wa huduma za usafiri na Shirika la Ndege la
Seychelles likiongoza kwa Bara Hindi.
0 comments:
Post a Comment