Tuesday, 12 April 2016

HAKIMU ‘FEKI’ ATIWA MBARONI…

Mkazi wa kijiji cha Kanyama Kata ya Bujora Wilaya ya Magu mkoani Mwanza Erick Mkundi (23), ametiwa mbaroni kwa tuhuma za kufanya kazi kama Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Kongoro akiwa hana sifa hiyo.

Mtuhumiwa huyo anadaiwa kuifanya kazi hiyo kuanzia Januari hadi Aprili 6 mwaka huu alipobainika, baada ya kushindwa kujitambulisha kwa Hakimu Mfawidhi wa wilaya hiyo Edmund Kente, kuwa ni hakimu na bila kuonyesha nyaraka zozote zinazomthibitisha kuwa taaluma hiyo.
Aidha ilidaiwa kuwa Mkundi alijikabidhi katika mahakama hiyo na kuanza kuendesha kesi, na hadi anatiwa mbaroni tayari alishatoa hukumu kwa washtakiwa wanne na wengine kadhaa kuwasotesha mahabusu.
Mmoja wa watumishi wa mahakama hiyo aliyeomba jina lake lisitajwe kwa madai kuwa si msemaji, alieleza kuwa walifanya kazi na Mkundi kwa miezi minne wakiamini kwamba ni mtumishi halali wa Idara ya Mahakama.
Akilithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Wilaya ya Magu Charles Mkapa, amesema Mkundi alikamatwa baada ya polisi kupewa taarifa zake za kufanya kazi bila kibali.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza Francis Kabwe, alipoulizwa kuhusiana na tukio la hakimu huyo feki, alisema hajapata taarifa kamili lakini atalizungumzia suala hilo leo.

Related Posts:

0 comments:

Post a Comment