Monday 4 April 2016

UJERUMANI YAKABIDHI NDEGE KUKABILI UJANGILI…

Serikali ya Ujerumani imetoa msaada wa ndege maalumu aina ya “Husky A-1C Aircraft” kwa Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Malisili na Utalii kusaidia katika doria za kupambana na ujangili katika Pori la Akiba la Selous.

Msaada huo wenye thamani ya Euro 200,000 sawa na Sh milioni 498.2 umekabidhiwa kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Serikali ya Shirikisho la Ujerumani, Dk Gerd Muller katika hafla fupi iliyofanyika Matambwe ndani ya Pori la Akiba la Selous.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na maofisa wa Ubalozi wa Ujerumani nchini wakiongozwa na Balozi Egon Konchanke, viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) na mashirika ya Maendeleo ya Kimataifa ya FZS, WWF, GIZ na KFW.
Akizungumza katika hafla hiyo, Profesa Maghembe alisema ndege hiyo itasaidia jitihada za Serikali za kupambana na ujangili kwa kufanya doria katika anga ya Pori la Akiba la Selous na kusaidia kutoa taarifa za kiuhalifu pale itakapobainika na kuchukuliwa hatua stahiki za kukabiliana na uhalifu huo.

Kwa upande wake Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Ujerumani, Dk Muller alimueleza Profesa Maghembe kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza uhifadhi nchini.

0 comments:

Post a Comment