Friday 1 April 2016

AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUTISHIA KUMUUA RAIS MAGUFULI….

Kondakta Hamimu Seif (42) mkazi wa Mwananyamala Ujiji jijini Dar es Salaam, amefikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu shitaka kumtishia kumuua kwa maneno Rais Dk. John Magufuli kwa kujitoa mhanga.
Wakili wa Serikali Keneth Sekwao alidai kuwa Machi 10 mwaka huu katika baa ya Soweto iliyopo Kijitonyama Wilaya ya Kinondoni, mshtakiwa alimtishia kumuua Rais Dk.Magufuli kwa kujitoa mhanga.
Ilidaiwa kuwa mshtakiwa alitamka kwa kusema kuwa,kwa haya mambo anayoyafanya Rais Dk. Magufuli yupo tayari kujilipua kwa kujitoa mhanga ili kumwangamiza.

Mshtakiwa huyo alisomewa shitaka lake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hellen Riwa, hata hivyo alikana shitaka hilo na upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Hakimu Riwa alimtaka mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini hati ya dhamana yenye thamani ya Sh. milioni mbili kila mmoja.

Hata hivyo, mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti hayo na kupelekwa mahabusu hadi Aprili 14, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

0 comments:

Post a Comment