Muuguzi anayefanya kazi Kituo cha
Afya Kata ya Igurubi Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Damian Mgaya (26)
anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma ya kumbaka binti wa miaka 18 mkazi wa
kitongoji cha Mwagala B, Kijiji cha Mwagala.
Mtendaji wa
Kata ya Igurubi, Ntemi James alisema uhalifu huo umefanyika Julai 14, mwaka huu
saa 8 hadi alfajiri wakati binti huyo akimuuguza mama yake, Tatu Simbi ambaye
amelazwa katika kituo hicho cha afya baada ya kushambuliwa kwa kipigo na mume
wake. James alidai mtuhumiwa alimpokea mama wa binti huyo akiwa hoi na ndipo
alimpatia matibabu kisha kumlaza katika kituo hicho cha afya huku akimchoma
sindano ya usingizi ambayo ilisababisha mama huyo kupitiwa na usingizi.
Mtendaji huyo
alidai kuwa muuguzi Damian alipoona mama wa binti huyo amelala, alimwambia
waende wote chumba kingine ili akachukue dawa ya mama yake; lakini hata hivyo
hakumpa dawa na badala yake alimwambia amchome sindano ili asipate maradhi kwa
kuwa mazingira ya hospitali sio mazuri. Baada ya kuambiwa hivyo, binti huyo
alikubali kuchomwa sindano mbili na alipochomwa sindano ya kwanza aliishiwa
nguvu na alipochomwa sindano ya pili alianguka na kupitiwa na usingizi hadi
asubuhi.
Alisema baada
ya kuona amelala pasipokuwa na fahamu, muuguzi huyo alianza kumbaka hadi
alfajiri alipoamshwa na mama yake huku yeye akiwa hajitambui kutokana na
maumivu aliyokuwa akiyasikia sehemu zake za siri na mwili wote. Kaimu Mganga
Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Bonaventura Kalumbete alithibitisha kubakwa kwa binti
huyo na muuguzi huyo na kueleza kuwa baada ya kupata taarifa hiyo, alituma timu
ya wataalamu ambayo ilibaini binti huyo kubakwa na amelazwa kwenye kituo hicho
na hali yake ni mbaya kwani hawezi kutembea.
Aidha, Dk
Kalumbete alisema uchunguzi wa awali unaonesha binti huyo alichomwa sindano
wakati alikuwa hata haumwi na hizo dawa nazo zimechangia kumsababishia
kushindwa kutembea huku akiahidi kuwa baada ya uchunguzi, muuguzi huyo
atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Mkuu wa Wilaya
ya Igunga ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, John
Mwaipopo alikiri kukamatwa kwa muuguzi baada ya kupokea taarifa ya kubakwa kwa
binti huyo, alimwagiza Mkuu wa Polisi Igunga kumkamata muuguzi huyo Damian
Mgaya ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
0 comments:
Post a Comment