Monday, 3 July 2017

SAMSUNG YATUMIA SEHEMU ZA NOTE 7 KUUNDA SIMU MPYA…..

Kampuni ya mawasiliano ya Samsung imeanza kuuza simu nyingine ambazo inasema imetumia baadhi ya sehemu na vipande vilivyokuwa kwenye simu za Galaxy Note 7 ambazo zilikumbwa na matatizo.

Simu hizo za Galaxy Note 7 zilikuwa zinashika moto na kulipuka kutokana na tatizo kwenye betri zake.
Kampuni hiyo imesema simu hizo mpya kwa Kiingereza Note Fan Edition zitapunguza athari za kimazingira kutoka kwa mabaki ya simu hizo ambazo ziliacha kuuzwa kutokana na hitilafu hizo.
Simu hizo mpya zitauzwa Korea Kusini pekee na zitaanza kuuzwa tarehe 7 Julai.
Kampuni hiyo imesema simu hizo zitakuwa na betri ndogo ambazo ni salama zaidi kuliko simu hizo za awali.
Samsung iliacha kuunda simu za Galaxy Note 7, ambayo ilifaa kuisaidia kampuni hiyo kushindana na simu mpya za iPhone, mwishoni mwa mwaka jana baada ya kwanza kuwaomba wateja wazirejeshe nzifanyiwe ukarabati lakini hatua hiyo ikakosa kufaulu.
Inakadiriwa kwamba simu 2.5 milioni zilirejeshwa kwa kampuni hiyo.
Simu hiyo mpya itakwua na vipande kutoka kwa simu ambazo zilirejeshwa na wateja na vipande vingine kutoka kwa simu za Samsung ambazo hazikuwa zimeuzwa.

Betri ndogo na bei nafuu

Watetezi wa mazingira wamekuwa wakiishinikiza Samsung kutumia tena baadhi ya sehemu za Galaxy Note 7 ili kupunguza taka ambazo zingetokana na simu hizo.
Inakadiriwa kwamba simu 400,000 mpya zitaanza kuuzwa kuanzia Ijumaa.
Bei yake itakuwa ni won 700,000 za Korea ($615; £472), ambayo ni 30% chini ya bei iliyokuwa ya Galaxy Note 7.
Simu hizo zitakuwa na betri za 3,200 mAh na Samsung wanasema betri hizo zimechunguzwa vyema.
Note 7 zilitumia betri za nguvu ya 3,500 mAh.

Simu za Samsung Galaxy Note 8, ambazo zitatolewa kuifuata Note 7, zinatarajiwa kuanza kuuzwa baadaye mwaka huu.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment