Nyama nyekundu ni kitoweo kitokanacho na wanyama. Mbali na wanyama wa porini, watu wengi hupata nyama hiyo kutokana na kuchinja wanyama wafugawao kama ng’ombe, mbuzi, kondoo na ngamia.
Nyama nyekundu hutakiwa kuandaliwa kwa umakini iwe salama na bora kwa afya ya mlaji tofauti sana na inavyoandaliwa mara nyingi na Watanzania wengi.
Ofisa Mifugo Bodi ya Nyama Tanzania Ezekiel Maro anasema kuwa, nyama bora na salama inayotakiwa kuliwa ni iliyochinjwa na kuwekwa katika chumba chenye baridi (chilling) kuanzia saa nane hadi 24 kuruhusu misuli kufa na kutengeneza nyama.
Anasema nyama inayoliwa na wengi huwa ni msuli kutokana na kutokaa saa nane hadi 24 kabla ya kuliwa.
Akizungumza kwenye maonesho ya 41 ya Biashara ya Kimataifa DITF Maro anasema zipo athari za nyama inayoliwa kabla ya kukaa muda huo. Athari hizo anasema ni pamoja na kuwa na kiasi kikubwa cha tindikali, kukosa ulaini pamoja na ladha.
Akizungumzia kuhusu hali ya ulaji wa nyama nchini, mtalaamu huyo anasema mtanzania anakula wastani wa kilo 15 za nyama kwa mwaka wakati kiwango halisi kinachotakiwa ni kilo 50 kwa mwaka.
Hivyo anasema wananchi wanapaswa kufahamu kuhusu ulaji wa nyama bora na salama, waelewe kuhusu biashara ya nyama namna inavyofanyika na pia waelewe majukumu ya Bodi ya Nyama.
0 comments:
Post a Comment