Saturday 19 August 2017

POLISI WAANZISHA MSAKO MKALI KUWATAFUTA WALIOMUUA WAYNE LOTTER……….

Jeshi la Polisi nchini Tanzania linaendelea na msako mkali kuwatafuta watu waliompiga risasi na kumuua Mkurugenzi na Mwanzilishi-Mwenza wa Shirika lisilo la kiserikali la PAMS Foundation, Wayne Lotter jijini Dar es Salaam juzi.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari nchini Tanzania Lotter ndiye aliyekuwa amewezesha kukamatwa kwa mfanyabiashara, Yang Feng Glan maarufu kama ‘Malkia wa Meno ya Tembo’ hivi karibuni baada ya mhalifu huyo kusakwa kwa muda mrefu katika mataifa mbalimbali duniani kwa kuhusika na biashara ya meno ya tembo.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne Maghembe ameeleza kusikitishwa na tukio hilo la mauaji hayo ya mwanaharakati huyo.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Kamanda Kanda Maalumu, Lucas Mkondya amesema tukio hilo lilitokea Agosti 16, saa tano maeneo ya makutano ya barabara ya Haile Selassie na Kaole eneo la Masaki.
Taarifa kutoka eneo la tukio zinasema Lotter (miaka 51), alipigwa risasi katika maeneo hayo ya Masaki, wakati akitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) ambapo teksi aliyopanda ilisimamishwa na gari lingine kabla ya watu wawili kuteremka na kumpiga risasi.
Lotter alikuwa Mkurugenzi na Mwanzilishi-Mwenza wa PAMS Foundation, Shirika lisilo la Kiserikali ambalo linajihusisha na masuala ya kupinga ujangili ambalo lilianza shughuli zake Tanzania mwaka 2009.
Duru za harakati za kulinda mazingira zimeeleza kuwa Lotter alikuwa amepanga kufanya mikakati mbalimbali ya kukabiliana na ujangili wa tembo ikiwemo kuzindua vilabu vya kupinga ujangili, kufunga vifaa vya GPS kwa tembo wote nchini, pia alikuwa msaada kwa serikali kupitia miradi mbali mbali kama vile kufanikisha kumkamata malkia wa ndovu aliyekuwa anatafutwa Dunia nzima ambaye alikamatwa nchini miezi michache iliyopita.
Pia alianzisha vikosi vya ulinzi (game rangers) ambao aliwalipa ili kusaidia ulinzi wa tembo kwenye mbuga mbalimbali nchini. Alifadhili pia filamu ya The Ivory Game iliyochezewa Tanzania na China, ambayo ilizinduliwa Hollywood, Marekani ikionesha ujangili unavyofanyika na pia alisaidia magari ya doria kwa Jeshi la Polisi na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Polisi imesema wauaji hao wanaodhaniwa kuwa ni majambazi mbali na kumuua mkuregenzi huyo, walipora kompyuta mpakato tatu, simu moja aina ya Nokia na nyaraka mbalimbali.

0 comments:

Post a Comment