Serikali ya Brazil imefutilia mbali hifadhi kubwa ya taifa katika eneo la
Amazon ili kutoa fursa ya uchumbaji wa madini katika eneo hilo.
Hifadhi hiyo, yenye
ukubwa wa kilomita 46,000 mraba (maili mraba 17,800) hupatikana katika majimbo
ya kaskazini ya Amapa na Para na inaaminika kuwa na dhahabu pamoja na madini
mengine.
Serikali imesema
maeneo tisa ya uhifadhi na ardhi inayolindwa ya watu asilia, ambayo
yanapatikana ndani ya hifadhi hiyo, yataendelea kulingwa kisheria.
Lakini wanaharakati wa
hutetea uhifadhi wa utamaduni na mazingira wamelalamika kwamba maeneo hayo
yataathirika pakubwa.
Kwa jumla, inakadiriwa
kwamba 30% ya eneo lote la hifadhi hiyo litatumiwa kwa uchimbaji wa madini.
Agizo rasmi kutoka kwa
Rais Michel Temer lilifutilia mbali hifadhi hiyo ambayo hufahamika kama Hifadhi
ya Taifa ya Shaba Nyekundu na Washirika (Renca).
Maurício Voivodic,
mkuu wa shirika la uhifadhi wa wanyama la WWF nchini Brazil, alitahadharisha
mwezi jana kwamba uchimbaji wa madini katika eneo hilo utasababisha
"ongezeko kubwa la watu, ukataji mkubwa wa miti, kuharibiwa kwa chemchemi,
kupotea kwa viumbe na miti pamoja na kuzuka kwa mizozo kuhusu ardhi".
Wizara ya madini na
nishati nchini Brazil ilipendekeza kufutwa kwa hifadhi hiyo ili kuchochea
maendeleo eneo hilo.
Kwa mujibu wa ripoti
ya WWF, eneo kuu ambalo litatumiwa kwa uchimbaji wa madini ya shaba nyekundu na
dhahabu litakuwa ndani ya eneo moja miongoni mwa maeneo yanayofaa kulindwa,
ambalo huitwa Hifadhi ya Viumbe ya Maicuru.
Inasadikika kwamba kuna dhahabu pia katika msitu wa Para,
ambao unapatikana ndani ya hifadhi hiyo.
WWF wanasema kuna uwezekano wa
kuzuka kwa mizozo katika hifadhi mbili za watu asilia ambazo ni makao ya jamii
ambazo zimekuwa zikiishi bila kuingiliwa na watu kutoka nje.
Ripoti ya WWF imesema 'mbio za
kukimbilia dhahabu' eneo hilo zinaweza kuharibu utamaduni wa watu hao.
0 comments:
Post a Comment