Friday, 25 August 2017

WENYE VVU WAKITUMIA VIZURI ARVS HAWAWEZI KUAMBUKIZA...

Wenye Virusi Vya Ukimwi (VVU) wanaotumia dawa za kufubaza virusi (ARVs), wamethibitika kitaalamu kuwa wakitumia dawa hizo kwa uaminifu bila kukatisha dozi, hawawezi kuwaambukiza watu wengine kwa kujamiiana.

Isipokuwa maambukizi yanawezekana endapo mtu huyo anayetumia dawa akijikata na damu ikadondokea kwenye kidonda au eneo lenye mchubuko la mtu asiyekuwa na virusi.
Hata hivyo Ofisa Mkuu wa Uendeshaji wa taasisi ya kimataifa inayojihusisha masuala ya afya ya Management and Development for Health (MDH), Dk Nzovu Ulenga amehimiza utumiaji wa dawa hizo kwa uaminifu, akisema dozi ikikatishwa, ndani ya siku 30 virusi vinaibuka tena na maambukizi kwa wengine yanaendelea kama kawaida.
Dk Ulenga alitoa taarifa hiyo jana kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ukimwi ya Bunge, kwenye kikao cha kupokea na kujadili taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi mikubwa ya PEPFAR na Global Fund inayotekelezwa na asasi zisizo za kiserikali nchini.

Dk Ulenga alikuwa akifafanua hoja na maswali ya wajumbe wa kamati juu ya matumizi ya ARVs.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment