Tuesday 17 March 2015

Unajua kwa nini unapiga mihayo...



Kwa kawaida upigaji wa miayo huashiria kuchoka kwa mwili, akili au kujisikia kuchoshwa na jambo au hali fulani. Hali hii hutokea bila kutarajia wala haiepukiki, kama ilivyo kuhema. 

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa kuhusu miayo, binadamu huanza kupiga miayo tangu akiwa tumboni na umri wa wiki 11!

Kuna maelezo mengi tofauti kuhusu suala la kupiga miayo, lakini yanayovutia zaidi ni yale yanayofanywa na mtafiti wa Chuo Kikuu cha Princeton Marekani ambaye amegundua 

kuwa kitendo cha kupiga miayo huwa kinafanya kazi muhimu sana ya kuupoza ubongo.

Utafiti huo unasheheresha kwa kusema kuwa miayo huwa sawa na ‘reguleta’ ya kurekebisha joto la ubongo, pale joto linapokuwa limezidi kwenye ubongo kutokana na sababu mbalimbali, miayo hutokea kuupoza.

Imeelezwa kuwa watu wengi hupiga miayo wakati wa kipindi cha baridi kuliko kipindi cha joto kwa sababu kipindi cha baridi ubongo huchemka na kitendo cha kupiga miayo huwa kinatokana na mahitaji ya mwili ya kiasili ya kurekebisha hali ya joto kwenye ubongo.

Vile vile utafiti umeonesha kuwa binadamu anapokosa usingizi usiku, joto la ubongo huongezeka kutokana na kufikiri, hivyo anapoamka asubuhi hujikuta analazimika kupiga miayo ili kurekebisha joto lililozidi wakati huo.

Ubongo hufanya kazi kama kompyuta, ambayo hufanyakazi vizuri zaidi inapokuwa imepoa, hivyo maumbile ya kiasili hufanyakazi yake ya kujiendesha yenyewe pale kiungo chochote cha mwili kinapoonekana kuhitaji msaada.

Hata hivyo, utafiti mwingine unaonesha kwamba kupiga miayo kupita kiasi, kunaweza kuwa ni dalili ya tatizo lingine la kiafya, linalosababisha kuongezeka kwa joto kwenye ubongo au kuharibika kwa mfumo wa fahamu.

Kwa upande mwingine, kupiga miayo huwa ni dalili ya mabadiliko ya kimwili, kutoka hali ya uchangamfu kwenda uchovu au usingizi au kinyume chake. Kwa mujibu wa mwanasayansi wa Chuo Kikuu cha Maryland, Marekani, Dk. Robert Provineix, ni sawa pia kusema kuwa utafiti zaidi unahitajika ili kujua nini husababisha binadamu na wanyama wengine kupiga miayo.

Wakati mwingine, upigaji wa miayo mfululizo, huweza kuwa ni dalili ya matatizo ya moyo. Unapokutwa na hali kama hiyo mara kwa mara ni vyema ukaenda kuonana na daktari na kufanyiwa vipimo zaidi. 

Vile vile upigaji wa miayo mfululizo huweza kuwatokea wagonjwa wa kifafa, muda mfupi kabla ya kushikwa na kuanguka.Hivyo ni vyema kujitambua kama miayo unayopiga ni ya kawaida au siyo. Kwa sababu inawezekana kuwa ni dalili ya tatizo lingine kubwa la kiafya.  



0 comments:

Post a Comment