Friday 27 March 2015

Utafiti: Hali ya uchumi ya mtu mmojammoja nchini ni mbaya kuliko ilivyokuwa miaka 10 iliyopita..!!!

Hivi karibuni, Taasisi ya Repoa ilitoa utafiti wake unaoonyesha kuwa hali ya kiuchumi ya wananchi inazidi kuwa mbaya ikilinganishwa na ilivyokuwa miaka 10 iliyopita.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa, licha ya pato la taifa kuendelea kuongezeka hadi kufikia asilimia saba, Watanzania wengi wanaamini kwamba hali ya uchumi nchini mbaya.
Utafiti huo wa Afrobarometer, awamu ya sita uliofanywa kati ya Agosti 26 na Septemba 29 mwaka jana, walihojiwa Watanzania 2,386 wa Tanzania Bara na Visiwani.
Wananchi hao walisema kuwa hali ya maisha inazidi kuwa mbaya ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 2003.
Akitoa ripoti ya utafiti huo, Dk Lucas Katera kutoka Repoa, anasema wananchi wanalalamika kuwa licha ya Serikali kusema kuwa uchumi ni mzuri na kwamba nchi inapiga hatua ikilinganishwa na ilivyokuwa, wanaona watu wachache tu ndiyo wanaonufaika na maendeleo hayo.
Akitoa mfano anasema mwaka 2003 asilimia 42 walisema hali ya uchumi ilikuwa mbaya, mwaka 2005 asilimia 38, utafiti uliofuata mwaka 2008 idadi ya wananchi iliongezeka na kufikia asilimia 57 huku mwaka jana walikuwa asilimia 67.
Mtafiti huyo anasema matokeo hayo yamebaini kuwa kuna uhusiano wa karibu kati ya hali mbaya ya kiuchumi na utoaji mbaya wa huduma za jamii.
Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Prosper Ngowi anasema uchumi unaweza kukua, lakini kama hakutakuwa na matumizi sahihi ya fedha za umma wananchi wataendelea kuona kasoro za kiuchumi.

0 comments:

Post a Comment