Kwa kawaida upigaji wa miayo
huashiria kuchoka kwa mwili, akili au kujisikia kuchoshwa na jambo au hali
fulani. Hali hii hutokea bila kutarajia wala haiepukiki, kama ilivyo kuhema.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa kuhusu miayo, binadamu huanza kupiga miayo
tangu akiwa tumboni na umri wa wiki 11!
Kuna maelezo mengi tofauti kuhusu suala la kupiga miayo, lakini yanayovutia
zaidi ni yale yanayofanywa na mtafiti wa Chuo Kikuu cha Princeton Marekani
ambaye amegundua
kuwa kitendo cha kupiga miayo huwa kinafanya kazi muhimu sana
ya kuupoza ubongo.
Utafiti huo unasheheresha kwa kusema kuwa miayo huwa sawa na ‘reguleta’ ya
kurekebisha joto la ubongo, pale joto linapokuwa limezidi kwenye ubongo
kutokana na sababu mbalimbali, miayo hutokea kuupoza.
Imeelezwa kuwa watu wengi hupiga miayo wakati wa kipindi cha baridi kuliko
kipindi cha joto kwa sababu kipindi cha baridi ubongo huchemka na kitendo cha
kupiga miayo huwa kinatokana na mahitaji ya mwili ya kiasili ya kurekebisha
hali ya joto kwenye ubongo.
Vile vile utafiti umeonesha kuwa binadamu anapokosa usingizi usiku, joto la
ubongo huongezeka kutokana na kufikiri, hivyo anapoamka asubuhi hujikuta
analazimika kupiga miayo ili kurekebisha joto lililozidi wakati huo.
Ubongo hufanya kazi kama kompyuta, ambayo hufanyakazi vizuri zaidi inapokuwa
imepoa, hivyo maumbile ya kiasili hufanyakazi yake ya kujiendesha yenyewe pale
kiungo chochote cha mwili kinapoonekana kuhitaji msaada.
Hata hivyo, utafiti mwingine unaonesha kwamba kupiga miayo
kupita kiasi, kunaweza kuwa ni dalili ya tatizo lingine la kiafya,
linalosababisha kuongezeka kwa joto kwenye ubongo au kuharibika kwa mfumo wa
fahamu.
Kwa upande mwingine, kupiga miayo huwa ni dalili ya mabadiliko
ya kimwili, kutoka hali ya uchangamfu kwenda uchovu au usingizi au kinyume
chake. Kwa mujibu wa mwanasayansi wa Chuo Kikuu cha Maryland, Marekani, Dk.
Robert Provineix, ni sawa pia kusema kuwa utafiti zaidi unahitajika ili kujua
nini husababisha binadamu na wanyama wengine kupiga miayo.
Wakati mwingine, upigaji wa miayo mfululizo, huweza kuwa ni
dalili ya matatizo ya moyo. Unapokutwa na hali kama hiyo mara kwa mara ni vyema
ukaenda kuonana na daktari na kufanyiwa vipimo zaidi.
Vile vile upigaji wa
miayo mfululizo huweza kuwatokea wagonjwa wa kifafa, muda mfupi kabla ya
kushikwa na kuanguka.Hivyo ni vyema kujitambua kama miayo unayopiga ni ya
kawaida au siyo. Kwa sababu inawezekana kuwa ni dalili ya tatizo lingine kubwa
la kiafya.