Thursday 25 June 2015

Akamatwa uwanja wa ndege Dar na kobe 173…


Jeshi la Polisi Uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere,linamshikilia raia wa Kuwait Hussein Mansoor, kwa kukutwa na kobe hai 173 aliokuwa akiwasafirisha kueleka nchini kwake.

Kaimu Mkurugenzi wa Uwanja wa JNIA Clemence Jingu, amesema abiria huyo alikamatwa usiku wa kuamkia jana akijitayarisha kupanda ndege ya Emirates iliyokuwa ikielekea Kuwait kupitia Dubai.
Jingu amesema raia huyo alikamatwa saa tano usiku katika eneo la abiria wanaoondoka, baada ya polisi wa uwanja huo kwa kushirikiana na maofisa wa Wizara ya Maliasili, kufanya ukaguzi na kugundua kobe hao wakiwa wamefichwa kwenye masanduku makubwa mawili.
Jingu amesema kobe hao wenye thamani ya Sh 30 milioni,ni miongoni mwa nyara muhimu za Serikali ambazo zimekuwa zikitaifishwa kupitia mbinu mbalimbali.
Kamanda wa Polisi wa uwanja huo Khamis Suleiman, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa, mtuhumiwa huyo anashikiliwa na jeshi hilo kwa uchunguzi zaidi.
Tukio hilo lilithibitishwa pia na Kamishna wa Interpol Tawi la Tanzania Gustav Babile,ambaye amesema raia huyo alikamatwa na wanyama hao huku akiwa na vibali halali.

Tukio hili linafanana kwa kiasi kikubwa na lile lililotokea Januari 8 mwaka huu, ambapo raia mwingine wa Kuwait Ahmed Ally Mansour, alikamatwa katika uwanja huo akiwatorosha kenge hai 149 wenye thamani ya Sh 6.3 milioni.

0 comments:

Post a Comment