Serikali ya
Marekani imethibitisha habari ya kudukuliwa taarifa za karibu wafanyakazi
milioni nne wa serikali ya nchi hiyo.
Shirika la habari
la Ufaransa limeinukuu serikali ya Marekani ikisema kuwa,wadukizi katika
mitandao ya Intaneti wamedukiza taarifa za karibu wafanyakazi milioni nne wa
zamani na wa hivi sasa wa serikali ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa
ripoti hiyo idara ya masuala ya wafanyakazi ya Marekani, mwezi Aprili mwaka huu
iligundua kuwa, taarifa za wafanyakazi milioni nne wa serikali ya nchi hiyo
zimedukuliwa.
Ripoti hiyo
imeongeza kuwa, hadi sasa haijajulikana iwapo wafanyakazi wa ngazi za juu wa
Marekani ni miongoni mwa watu waliodukuliwa taarifa zao au la.
Gazeti la
Washington Post limewanukuu viongozi wa serikali ya Marekani wakidai kuwa,
wadukizi kutoka China ndio waliofanya udukizi huo.
Hata hivyo ubalozi
wa China mjini Washington umekanusha vikali madai hayo,na kusema kuwa kauli
hizo za viongozi wa Marekani ni za kukurupuka.
Msemaji wa ubalozi
huo Zhu Haiquan amesema kuwa, China inafanya juhudi kubwa za kupambana na
udukizi mitandaoni, na kwamba si jambo jepesi kuweza kufuatilia na kugundua
matukio kama hayo ambayo yanafanyika ndani ya mipaka ya nchi nyingi duniani.
0 comments:
Post a Comment