Wednesday, 17 June 2015

Wanafunzi Somalia wafanya mtihani wa taifa baada ya miaka 25..!!!

Mtihani wa kwanza Somalia katika miaka 25
Zaidi ya wanafunzi elfu 70 walifanya mitihani ya kidato cha nne katika maeneo ya kusini na kati
mwa Somalia, ikiwa ni mitihani ya kwanza ya kitaifa katika kipindi cha miaka 25.

Mitihani hiyo itaendelea kwa muda wa siku tano zijazo.
Katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu, vituo 11 vilianzishwa kuwawezesha watahiniwa kufanya mitihani.
Elimu ni mojawapo ya sekta zilizoathirika vibaya na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza nchini Somalia mwaka wa 1991.
Tangu kusambaratika kwa serikali kuu nchini Somalia, mitaala mbali mbali imetumika katika shule na kufunzwa katika lugha tofauti tofauti.
Sasa wizara ya elimu inasema imechukuwa hatua za kuunganisha mitaala hiyo na kuhakikisha kuwa wanafunzi kote nchini wanafanya mtihani mmoja wa kitaifa.
Licha ya pingamizi kutoka kwa makundi mbali mbali yaliyoyounda mitala hiyo katika shule za kibinafsi nchini Somalia, serikali iliidhinisha kufanyika kwa mitihani huu.
Waziri wa elimu wa Somalia Khatra Bashir Ali ambaye alikuwa miongoni mwa maafisa waliosimamia mitihani hiyo, alisema nchi hiyo ina mengi ya kufanya katika ulimwengu wa sasa unaoegemea mfumo wa digitali.
Wengi wa wanafunzi waliofanya mitihani hiyo walikuwa na furaha.
Walisema wamefurahishwa na hatua ya kufanya mitihani iliyopangwa na kuandaliwa na serikali kinyume na hapo awali ambapo wasimamizi wa shule kibinafsi ndio waliochukuwa jukumu hilo.
Ulinzi umeimarishwa huku wasimamizi wakiwapekua wanafunzi ilikuhakikisha hakuna udanganyifu.

Kwa wasomali hii bila shaka ni hatua muhimu ya kihistoria katika juhudi za kujaribu kujenga upya taifa ambalo limezongwa na miongo miwili ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

0 comments:

Post a Comment