Askofu Josef Weslowski kushtakiwa kwa kudhulumu watoto |
Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis, ameonekana kuanza kuwakabili makasisi waliotuhumiwa kwa sakata ya ngono.
Askofu mmoja aliyekua mjumbe wa papa
katika jamhuri ya Dominican,atafikishwa mahakamani Julai 11.
Josef Weslowski raia wa Poland,ametuhumiwa
kuwaharibu watoto wa kiume pamoja na kuwa na sinema chafu za watoto.
Kwingineko maaskofu wawili wa
Marekani wamejiuzulu, kwa kukosa kuwalinda watoto ambao walidhulumiwa kimapenzi
na makasisi.
Mwanadiplomasia huyo wa zamani amekuwa
katika kifungo cha ndani huko Vatican, tangu alipovuliwa wadhfa aliokuwa
amepewa na kurudishwa kutoka Jamhuri ya taifa la Dominican mwaka wa 2013.
Sasa atakabiliwa na kesi kwa mujibu wa sheria mpya
zilizoidhinishwa na Papa Francis.
Hii inamaanisha kuwa anaweza
kupewa kifungo cha hadi miaka 12 jela iwapo atapatikana na hatia .
Askofu mwengine wa kanisa la
Mtakatifu Paulo huko Minnesota Marekani pamoja na msaidizi wake,nao walijiuzulu
baada ya kushtakiwa kwamba walishindwa kuchukua hatua dhidi ya kasisi mmoja
aliyeripotiwa kumnyanyasa mtoto kingono katika jimbo lake.
Papa Francis na viongozi
waliomtangulia wamekuwa wakishtumiwa vikali kwa kukosa kuwachukulia hatua au
hata kuwaondoa mamlakani,makasisi wanaoripotiwa kwenda kinyume na maadili na
hasa unyanyasaji wa kingono .
Mapema mwezi huu Papa Francis
aliunda tume maalum iliyopewa mamlaka ya kusikiliza na kuhukumu maaskofu
wanaotuhumiwa kufumbia macho vitendo vya unyanyasaji wa kingono ambayo huenda
vinaendelea katika makanisa yao.
Kwa namna hiyo inavyoelekea ni
kwamba Papa Francis angependa mashtaka dhidi ya watumishi wa makanisani
yashughulikiwe na mahakama maalum ya kanisa badala ya kesi hizo kupelekwa kwa
mahakama za kawaida za umma.
0 comments:
Post a Comment