Friday 10 April 2015

Mtanzania anayetuhumiwa kwa ugaidi Kenya kizimbani.

Mtanzania anayedaiwa kuhusika katika shambulizi la kigaidi lililoua watu 148 katika Chuo Kikuu cha Garissa-Kenya, Rashid Charles Mberesero,
jana alifikishwa mahakamani na kuwekwa kizuizini kwa mwezi mmoja wakati polisi wakiendelea kukusanya ushahidi dhidi yake.
Mtuhumiwa huyo ambaye pia anafahamika kwa jina la Rehani Dida alirejeshwa Nairobi kutoka Garissa alikopelekwa awali kwa ajili ya kuhojiwa baada ya kukiri kujihusisha na kundi la Al- Shabaab.
Mahakama jijini Nairobi ilisema jana kuwa mtuhumiwa huyo ambaye hakutakiwa kujibu tuhuma hizo na wenzake wanne watalazimika kuwa chini ya uchunguzi mkali wa polisi kwa kipindi cha mwezi mmoja na baadaye wanaweza kusomewa mashtaka ya kuhusika katika shambulizi hilo lililoua watu hao, wengi wao wakiwa ni wanafunzi.
Haikufahamika mara moja sababu za kuamuliwa kuwekwa kizuizini kwa muda huo mbali ya taarifa kueleza kuwa ‘watashikiliwa na polisi tena katika kituo cha siri’.

0 comments:

Post a Comment