Tuesday 7 April 2015

Kenya yashambulia ngome za al Shabab Somalia…



Ndege za jeshi la Kenya zimeshambulia kambi mbili za kundi la kigaidi la al Shabab nchini Somalia, ikiwa ni kulipiza kisasi cha kuuawa wanafunzi na wafanyakazi
wapatao 150 wa Chuo Kikuu cha Garissa kaskazini mwa Kenya.

Kanali David Obonyo Msemaji wa Jeshi la Kenya amesema kuwa, ndege za kivita za Kenya zimeshambulia kambi za kundi la kigaidi la al Shabab katika mkoa wa Gedo kaskazini mwa Somalia na kusababisha maafa makubwa kwenye kambi hizo.

Kanali Obonyo amesisitiza kuwa kambi hizo mbili za magaidi wa al Shabab zimeteketezwa kikamilifu.

Shambulio hilo la jeshi la Kenya limefanyika zikiwa zimepita siku tano tu, tokea kundi hilo liliposhambulia na kuua watu wanaokaribia 150 kwenye Chuo Kikuu cha Garissa, kilichoko umbali wa kilomita 150 kutoka kwenye mpaka wa nchi hiyo na Somalia.

Hivi karibuni kundi la al Shabab lilitishia kufanya mauaji mengine ya umati nchini Kenya na kusisitiza kwamba Wakenya watakabiliwa na mashambulio ya muda mrefu na ya kutisha.

Maeneo ya mashariki na kaskazini mwa Kenya yanayopakana na Somalia yamekuwa yakilengwa mara kwa mara na wanamgmabo wa al Shabab.

Kuanzia mwaka 2011 serikali ya Kenya ilipeleka wanajeshi wasiopungua elfu tatu kusini mwa Somalia kwa shabaha ya kupambana na kundi la kigaidi la al Shabab.

0 comments:

Post a Comment