Wednesday 29 April 2015

Utafiti mpya wabaini ‘Panya Road’ bado tishio Tz.

Vikundi vya uhalifu nchini vyenye muundo ‘Panya Road’ vinazidi kuwapa hofu wananchi kutokana na vitendo vyao vya kutishia amani, utafiti wa Taasisi ya kiraia ya Twaweza umebainisha.

Matokeo ya utafiti huo yaliyotolewa jana yalibainisha kuwa,watu wanane kati ya 10 (asilimia 84) wanaamini kuna uwezekano mkubwa wa kuathiriwa na vijana wahalifu.
Utafiti huo unaoitwa ‘Je tuko Salama?’ ulieleza kuwa wananchi watatu kati ya 10 wameshakumbana na wizi ndani ya kipindi cha mwaka jana, sawa na nusu ya Watanzania wote.
Takwimu za utafiti huo zilikusanywa kwa kuwahoji watu elfu 1 na mia 401 kutoka Bara, kati ya Februari na Machi mwaka huu.
Katika utafiti huo wananchi sita kati ya 10 (asilimia 60), walisema wamewahi kusikia kuhusu ‘Panya Road’ wakati wananchi tisa kati ya 10 (asilimia 87) walidai hakuna kikundi kama hicho katika maeneo yao.
Matokeo hayo yanabainisha zaidi kuwa wananchi bado wanaamini kuwa mfumo wa sheria haufanyi kazi ipasavyo.
Utaiti huo unaonyesha kuwa Zaidi ya nusu ya wananchi (asilimia 53) wanaamini kuwa raia wa kawaida ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria akitenda kosa, lakini kuadhibiwa kwa watu wenye kipato cha juu ni vigumu.
Lakini asilimia 14 wanaamini kuwa watu wenye kipato cha juu wanaweza kuadhibiwa iwapo watavunja sheria na wengine (asilimia 21) wanaona hilo pia linawezekana kwa watumishi wa umma, inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Hata hivyo utafiti huo umebainisha kuwa idadi hiyo imeshuka ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 2013.
Katika kipindi hicho asilimia 39 ya wananchi walidhani kuwa watumishi wa umma watakumbana na mkono wa sheria wakitenda kosa.
Pamoja na hayo yote wananchi sita kati ya 10 (asilimia 60), wanaamini Jeshi la Polisi linawahudumia zaidi watu wenye fedha kuliko wa kipato cha chini.
Utafiti huo wa maoni ya wananchi juu ya usalama na haki,ni sehemu ya mfululizo wa tafiti zitokanazo na mradi wa Sauti za Wananchi.

0 comments:

Post a Comment