![]() |
Waustralia wawili waliouawa |
Indonesia imetetea uamuzi wake wenye
utata wa kuamua kuwauwa walanguzi wanane wa dawa za kulevya wakiwemo
raia saba wa kigeni, ikisema kuwa hivyo ni vita dhidi ya biashara ya
mihadarati.
Kwa upande wake, Australia imemuita nyumbani balozi wake Nchini Indonesia, kama hatua ya kulalamikia kuuwawa kwa raia wake wawili waliohusika na ulanguzi huo.
Waziri mkuu Tony Abbott, anasema kuwa hata ingawa anaheshimu utawala wa Indonesia kama taifa huru, uhusiano wa mataifa hayo mawili hautaendelea kama kawaida kufuatia mauwaji ya wa-australia hao wawili.
Mkuu wa sheria Nchini Indonesia Muhammad Prasetyo, ameelezea hatua hiyo ya Ausralia kama hasira za muda mfupi tu.
![]() |
Moja ya majeneza ya wale waliouawa |
Licha ya vilio vya kuwasamehe watu hao kutoka kwa mataifa ya dunia,Indonesia iliamua kwa vyovyote kuwauwa.
Kuuwawa kwa mfungwa wa tisa raia wa Ufilipino, Mary Jane Veloso, kumecheleweshwa na Rais Joko Widodo, baada ya mwanamke mmoja kujiwasilisha kwa polisi nchini Ufilipino, akisema kuwa ndiye aliyemhadaa mfungwa huyo mwanamke mwenzake, kupeleka dawa za kulevya hadi Indonesia.
Brazil nayo inasema kuwa kuuwawa kwa raia wa pili wa Brazil Nchini Indonesia, katika kipindi cha miezi minne, ni hatua ya kutamausha na ambayo tayari imeyumbisha vibaya uhusiano wa kidiplomasia wa mataifa hayo mawili
0 comments:
Post a Comment