Monday 13 April 2015

Upungufu wa damu Hospitalini unavyochangia vifo vya uzazi...

Wakati ikiwa imebaki takribani miezi minane kabla ya kufikiwa kwa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDG) uhaba wa damu umekuwa kikwazo kupunguza vifo vya wajawazito na watoto katika hospitali ya mkoa wa Kagera.

Hospitali ya Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa taasisi za afya zilizoazimia kushiriki vyema katika kutekeleza Malengo ya Milenia, hasa lengo namba nne ambalo azma yake ni kupunguza kiwango cha theluthi mbili (2/3) cha vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano ifikapo 2015.
Pia hospitali hiyo imejizatiti kutekeleza lengo namba tano ambalo azma yake ni kupunguza kwa robo tatu wastani wa vifo vinavyotokana na uzazi ifikapo mwaka 2015.
Hata hivyo imeshindwa kupunguza vifo vya watoto na wanawake kutokana na ukosefu wa damu salama.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Kagera Juma Nyakina,anasema lengo la hospitali hiyo ni kuhakikisha vifo vya watoto wachanga na uzazi vinapungua hadi asilimia 60 au kuisha kabisa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, lakini inaonekana hawataweza kufikia lengo hilo, kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa damu salama.
Nyakina anasema huduma ya damu salama katika hospitali hiyo imekuwa kitendawili kutokana na kile kinachodaiwa ni ukosefu wa vitendanishi vya kupima sampuli za damu katika hospitali ya Kanda ya Bugando iliyopo Mwanza ambapo sampuli hizo hupelekwa kufanyiwa vipimo.
Nyakina anasema pamoja na mikakati ya kutekeleza malengo ya milenia bado vifo vya mama na watoto vinaendelea kutokea ambapo kwa kipindi cha mwaka 2014 watoto 166 wamekufai katika hospitali ya mkoa wa Kagera,kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ya upungufu wa damu na malaria.

0 comments:

Post a Comment