Wednesday 15 April 2015

Radi yaua wanafunzi 6 na mwalimu..


Watu nane wamefariki dunia na wengine 15 kujeruhiwa vibaya, baada ya kupigwa na radi ambayo chanzo chake kimeelezwa kuwa ni kunyesha kwa mvua kubwa iliyodumu kwa takribani saa tatu katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Taarifa za awali zimeeleza kuwa miongoni mwa watu waliofariki ni pamoja na wanafunzi sita, mwalimu mmoja na raia mmoja ambaye ni mkazi wa kijiji cha Bangwe mkoani Kigoma.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Dk Fadhili Kibaya ambaye ni Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Maweni amesema, Tukio hilo limetokea jana majira ya saa saba ambapo alipokea majeruhi 15 na miili 8 ikiwemo 6 ya wanafunzi, mwalimu mmoja wa shule ya msingi Kibilizi na mkazi mmoja wa Bangwe.
Shuhuda wa tukio hilo ambaye ni Mwalimu wa darasa la kwanza shuleni hapo  Melina Sililo, amesema wakati alipokuwa akiendelea na kufundisha aliona wingu likitanda na Mvua ikaanza kunyesha jambo lililosadabisha giza.
Amesema hali hiyo ilimfanya ashindwe kufundisha na wakati huohuo radi zilipigwa na moto ukatanda darasa zima ambapo yeye pamoja na watoto zaidi ya kumi walianguka.
Aidha amesema mwalimu Mbwambo alizimia kwa muda kidogo na baada ya kuhangaika kumpatia msaada walimkuta amekwisha fariki hali iliyowalazimu kuomba msaada wa gari la kuwafikisha maiti hao pamoja na majeruhi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo Maweni.

0 comments:

Post a Comment